Ijumaa, 15 Machi 2013

HILI HATULIFUMBII MACHO..

NANI ALIYEMTOBOA JICHO ABSALOM KIBANDA?

Na Mwandishi Wetu
SHAUKU ya kila Mtanzania ni kumjua nani au ni akina nani waliohusika katika kutekeleza tukio baya la kumshambulia hadi kumtoboa jicho Mhariri Mkuu wa New Habari Corporation, Absalom Kibanda.
 Absalom Kibanda akiwa na mkewe, Anjella Semaya, ndani ya ndege wakielekea nchini Afrika Kusini jana jioni.
Kibanda alikumbwa na tukio hilo usiku wa Februari 5, mwaka huu nje ya nyumba yake, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kibanda mwenyewe, awali alikuwa Sinza akiangalia mechi kati ya Real Madirid na Manchester United ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na baada ya hapo alirejea nyumbani kwake akiwa ndani ya gari lake.
Alisema alipofika nje ya geti kabla hajafunguliwa, walitokea watu asiowajua na kumshambulia hadi kumuachia majeraha sanjari na kumtoboa jicho la kushoto.
Mengi yameshasemwa kuhusu tukio hilo ambapo wengine wanasema waliolitekeleza ni majambazi, wapo wanaodai ni mambo binafsi lakini baadhi wana wasiwasi na mambo ya kisiasa.
Absalom Kibanda akiwa ICU.
MAJAMBAZI
Ni vigumu kuwaingiza majambazi au vibaka katika tukio hilo kwani akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa kwa matibabu, Kibanda mwenyewe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri alisema baada ya watu hao kumaliza kusudio lao hawakuondoka na kitu. Siku zote inajulikana, jambazi au kibaka huvamia mtu kwa kulenga kuondoka na kitu.
MAMBO BINAFSI
Watu wanaodai tukio hilo ni la mambo binafsi wanaweza kuwa na hoja, kwani ukweli wa madai hayo unaweza kuwa ndani ya nafsi ya Kibanda mwenyewe kwa vile ndiye anayejua anaishije na watu. Lakini kwa mujibu wa Kibanda mwenyewe, watu hao wakiwa wanamshambulia hakuna aliyekuwa akizungumzia lawama ya kisasi chochote cha  maisha yake ya kila siku.
Baadhi ya majeraha aliyoyapata Kibanda.
MAMBO YA KISIASA
Hapa ndipo penye sauti nyingi za wadau. Wengi wanasema siasa, hasahasa mchakato wa urais 2015 ndiyo umekuwa ukitajwa sana.
Mtu mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema:
“Unajua Kibanda aliwahi kuwa mhariri wa upande mwingine, akaondoka na sasa yupo kwa Bashe wa CCM. Inawezekana kuna watu wametumia nafasi hiyo, wameona kama amesaliti,” alisema mtu huyo.
Hata hivyo, mtu huyo alisema kuwa  pia Kibanda anaweza kuwa ameteswa na kambi za urais ndani ya chama kimoja cha siasa.
“Uchaguzi ni 2015, kwa vyovyote vile yeye kama mhariri atakuwa ana kambi yake, kwa hiyo kuna uwezekano ameshawahi kuandika habari iliyoathiri kambi nyingine, hilo nalo linawezekana. Lakini katika yote, tukio lake si la binafsi wala ujambazi,” alimalizia mtu huyo ambaye ana nafasi nzuri ndani ya chama tawala huku akisema serikali ina mkono mrefu, kila kitu kitakuwa wazi.
Gazeti hili linampa pole Kibanda na kumuombea kwa Mungu apone haraka - Mhariri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni